SERA YA LUGHA KATIKA ELIMU NA UKUZAJI WA KISWAHILI NCHINI UGANDA

Thesis Authors: I. Agume

Abstract

Kiswahili ni lugha ya Kibantu inayozungumzwa Afrika Mashariki. Hutafitiwa na hufundishwa katika nchi mbalimbali barani Afrika na nje. Itifaki ya Muungano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, inatambua Kiswahili kama lugha ya mawasiliano ya kikanda. Aidha, katiba ya nchi ya Uganda ya 1995 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2005, hati maalumu za serikali kama vile “The government white paper” ya 1992, zinatoa matamko bayana kuhusu uendelezaji wa Kiswahili nchini Uganda. Licha ya matamko ya kikatiba na mapendekezo kutoka hati mbalimbali za serikali, maendeleo ya Kiswahili nchini Uganda, hayajaenda sambamba na ya nchi nyingine za Muungano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Kwa hivyo, utafiti huu ulilenga kuchunguza mchango wa sera ya lugha ya elimu katika uendelezaji wa Kiswahili nchini Uganda. Utafiti huu uliongozwa na malengo yafuatayo: kujadili nafasi ya sera ya lugha katika ukuzaji wa Kiswahili kupitia mfumo wa elimu nchini Uganda, kufafanua changamoto zinazokumba ukuzaji wa Kiswahili kupitia mfumo wa elimu nchini Uganda na kufafanua suluhu za changamoto zinazokumba ukuaji wa Kiswahili kupitia mfumo wa elimu nchini Uganda. Data zisizo za kitakwimu zilikusanywa katika utafiti huu huku usampulishaji wa kimaksudi ukitumika kwa watafitiwa kumi na watatu kutoka taasisi za serikali na za binafsi jijini Kampala. Njia ya upekuzi wa nyaraka za maktabani na uchambuzi wa data za kiyaliyomo zilitumika. Aidha, mahojiano na maafisa kutoka taasisi zilizohusika yalifanywa. Hali kadhalika, Nadharia ya Upangaji Lugha ya Einer Haugen ilitumika katika utafiti huu. Matokeo ya utafiti yanaonyesha kuwa kuna nyaraka nyingi za sera, maagizo na matamko ambayo yanakipa Kiswahili hadhi ya kukuzwa na kuendelezwa kupitia mfumo wa elimu nchini Uganda. Hata hivyo, hali hii inakwamishwa na changamoto kama vile: ukosefu wa mikakati ya kutekeleza sera za lugha kuhusu Kiswahili, ukosefu wa utashi thabiti wa kisiasa, mvutano na mashindano kati ya lugha za kiasili na Kiswahili, mtazamo hasi kwa Kiswahili, serikali kutoajiri walimu wa kutosha wa Kiswahili na uhaba wa vifaa vya kufundishia shuleni. Suluhu za changamoto zinazokumba ukuzaji wa Kiswahili kupitia mfumo wa elimu zilizojadiliwa ni: serikali kuwekea mkazo utekelezaji wa sera kuhusu lugha ya Kiswahili, kuunda baraza la Kiswahili la kitaifa, kuhamasisha watu kwa wingi kuhusu manufaa ya Kiswahili, kuandaa warsha za kuboresha mbinu za ufundishaji kwa walimu wa Kiswahili, kuandaa na kutoa vifaa vya kutosha vya kufundishia na kujifunzia, kuthamini mtaala mpya wa sekondari unaozingatia umilisi na kuandaa vituo vya kujifunzia Kiswahili katika jamii. Matokeo ya utafiti huu ni muhimu kwa; watunga sera na wapangaji lugha, wakuza mitalaa na wadau wengine katika sekta ya elimu kuhakikisha utekelezaji wa mikakati mwafaka ya ukuzaji wa Kiswahili kupitia elimu. Utafiti huu pia unachangia maarifa yaliyopo kuhusu sera na mipango ya lugha pamoja na maendeleo ya Kiswahili nchini Uganda katika mipaka ya elimu. Isitoshe, matokeo ya utafiti huu yatakuwa msingi wa tafiti za baadaye kuhusu masuala ya sera ya lugha pamoja na maendeleo ya Kiswahili kupitia mawanda mengine kama utamaduni, bungeni, biashara na kwingineko.

 • 560 Views 39 Downloads

University Researchers

 • Projects

  TASNIFU - SHAHADA YA UZAMILI KATIKA KISWAHILI (CHUO KIKUU CHA MOI)

  Affiliation

  http://ir.mu.ac.ke:8080/jspui/handle/123456789/6372

  http://ir.mu.ac.ke:8080/xmlui/handle/123456789/6372

  https://scholar.google.com/scholar?hl=en&as_sdt=0%2C5&q=sera+ya+lugha+katika+elimu+na+ukuzaji+wa+Kiswahili&btnG=